Kesho Jumapili, March 1 2026 ni siku nyingine majira ya saa 2:15 usiku Tanzania itasimama kwa takribani dakika 90 wakati mpambano wa watani wa jadi kati ya Yanga dhidi ya Simba ukipigwa katika uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar.
Ni mchezo utakaozikutanisha timu mbili zenye mashabiki wengi zaidi nchini. Hii ikiwa mara ya pili timu hizo kukutana baada ya mchezo wa Ngao ya Jamii uliopigwa Septemba 16 mwaka jana Yanga ikichomoza kwa ushindi wa bao 1-0.
Bao pekee la Yanga katika mchezo huo lilifungwa na Pacome Zouzoua likiwa ni bao lake la tatu katika mechi za dabi ya Kariakoo.
Pacome anaungana na Maxi Nzengeli wakiwa ni wachezaji waliofunga mabao mengi zaidi kwenye mechi za dabi ya Kariakoo katika vikosi vya sasa vya Yanga na Simba.
Kesho nyota hao watakuwa wakisaka rekodi nyingine ya kibabe, endapo watafunga wataingia katika historia ya wachezaji waliofunga mabao mengi kwenye mechi za dabi muda wote.
Wote wamekuwa sehemu ya kikosi cha Yanga kilichoshinda mechi sita mfululizo dhidi ya Simba, wana nafasi ya kushuhudia ushindi mwingine wa saba dhidi ya watani wa jadi.