Kocha Mkuu wa Yanga Pedro Goncalves, ameonekana kupata mchanganyiko sahihi wa safu ya ushambuliaji baada ya kuanza kuwatumia pamoja washambuliaji wake wawili, Prince Dube na Laurindo Aurelio βDepuβ.
Ushirikiano wa wawili hao umeanza kuzaa matunda, huku wote wakionyesha makali makubwa ndani ya ligi na mashindano ya kimataifa.
Goncalves aliwaanzisha kwa pamoja katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Kabylie, ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-0. Depu alifunga mabao mawili katika mchezo huo, akiweka wazi uwezo wake wa kumalizia nafasi huku Dube akitoa asisti ya bao la tatu.
Wawili hao waliendelea kuanza pamoja kwenye mchezo wa Kombe la CRDB dhidi ya Cosmopolitan FC, lakini Dube alipata jeraha la kifundo cha mguu na kulazimika kutolewa wakati wa mapumziko.

Katika mchezo uliofuata wa ligi dhidi ya Namungo FC, Dube alikosekana. Ingawa Depu alifunga bao pekee la ushindi, Yanga haikuonyesha makali makubwa eneo la ushambuliaji kama ilivyokuwa walipocheza wote wawili.
Dube alirejea kikosini katika mchezo dhidi ya JKT Tanzania na kuanza sambamba na Depu, huku wote wakifunga mabao.
Kipindi cha kwanza Goncalves alianza na mfumo wa 4-4-2, akiwatumia kama washambuliaji wawili wa kati. Kipindi cha pili, baada ya kumuingiza Mohamed Damaro, alibadili mfumo kuwa 4-2-3-1, Dube akisogezwa upande wa winga wa kushoto.
Mikimbio ya Dube iliwapa wakati mgumu walinzi wa JKT Tanzania na kumwachia Depu nafasi ya kucheza kwa uhuru zaidi. Depu alifunga bao la pili akimalizia krosi ya Israel Mwenda.
Baada ya Depu kutolewa, Dube alirejea katikati kama mshambuliaji wa kati na kufunga bao akimalizia krosi ya Buba.
Kwa sasa, Dube na Depu kila mmoja ana mabao matano ya ligi, huku Depu akiweka rekodi ya kufunga katika kila mchezo wa ligi aliocheza hadi sasa, mabao matano katika mechi nne.
Muunganiko huo unaonekana kuwa silaha mpya ya Yanga msimu huu, huku mashabiki wakiamini kuwa kama wataendelea katika kiwango hiki, klabu hiyo itakuwa na nguvu zaidi katika harakati zake za kutetea ubingwa.