Mshambuliaji wa Yanga Clement Mzize msimu huu amekuwa na wakati mgumu kutokana na changamoto za majeraha.
Baada ya kukaa nje ya uwanja kwa takribani miezi mitatu Mzize alirejea uwanjani katika mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya AS FAR uliopigwa Morocco Wananchi wakipoteza kwa bao 1-0.
Mzize alitumika kwa takribani dakika 15 katika mchezo huo ambao ulikuwa mwanzo wa Yanga kuvuruga hesabu za kufuzu robo fainali baada ya kipigo.
Tangu wakati huo Mzize hakuonekana uwanjani katika mechi tatu zilizofuata ikielezwa amepata changamoto nyingine ya majeraha.
Kocha Mkuu wa Yanga Pedro Goncalves amekiri ni pigo kwa kikosi chake kuendelea kumkosa Mzize lakini jambo muhimu ni kuhakikisha anapona kabisa majeraha na kurudi uwanjanii akiwa yuko fit kwa asilimia 100.
“Mzize, amepata maumivu tena. Si kwa tatizo lile lile, ni jingine, madaktari wanapambana kuhakikisha anakuwa sawa. Jambo la muhimu ni kumuombea asiwe na jeraha kubwa litakalomfanya akae nje kwa muda mrefu tena,” alisema Goncalves wakati kikosi chake kilipokuwa kwenye maandalizi ya mchezo dhidi ya Namungo ambao ulipigwa jana na Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Changamoto za majeraha kwa Mzize zilianza wakati wa michuano ya CHAN 2024 akiumia wakati yuko kwenye majukumu ya timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars'.
Alirejea mwanzoni mwa msimu na akacheza mechi za hatua ya awali ligi ya mabingwa lakini baadae akalazimika kupelekwa Morocco kufanyiwa upasuaji wa goti.