Kumekuwa na maoni tofauti kutoka kwa mashabiki baadhi wakionesha kutofurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa Yanga licha ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Namungo Fc jana katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa uwanja wa Majaliwa.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa mabingwa hao watetezi Ali Kamwe amesema walifahamu mchezo dhidi ya Namungo Fc hautakuwa mwepesi na jambo muhimu ni kuwa wameondoka na alama tatu.
Kamwe amewataka mashabiki wa timu hiyo kuweka mawazo yao kwenye mchezo unaofuata dhidi ya JKT Tanzania akiweka wazi kuwa mchezo huo nao utakuwa mgumu.
"Unaelekea kwenye Dabi, halafu unacheza na Namungo inayofundishwa na kocha Juma Mgunda, ukipata alama tatu sema Alhamdulillah, wakubwa watakuwa wamenielewa."
"Bado tuna kibarua dhidi ya JKT Tanzania, hizi mechi mbili ni ngumu kuliko Derby yenyewe kwasababu zina macho ya watu wengi, ” alisema Kamwe.
Baada ya kuhitimisha mechi ya ligi ya mabingwa dhidi ya JS Kabylie pale visiwani Zanzibar Februari 15, siku tatu baadae Wananchi wakashuka dimba la KMC Complex kuikabili Cosmopolitan katika mchezo wa kombe la CRDB.
Juzi wakasafiri Ruangwa ambapo jana wakacheza dhidi ya Namungo Fc katika mchezo ambao walifanikiwa kuondoka na alama 3.
Wananchi wanarejea Dar leo ambapo Jumatano watakuwa kMC Complex kuwakabili vinara wa ligi hiyo, JKT Tanzania. Wakati Yanga ikipambana na ratiba ya bandika bandua, wapinzani wao JKT Tanzania wamepata muda wa kutosha kujiandaa na mchezo huo.
JKT Tanzania wana timu bora msimu huu na bila shaka watakwenda kuwapa Wananchi mechi ngumu siku ya Jumatano.
"Ratiba kwa sasa sio rafiki na hairuhusu mambo na mbwembwe nyingi zaidi ya pointi 3. Tuzipambanie hizi, Tuvuke kibingwa hapa."
"Kuelekea hizi dakika 90 za Jumatano ni ngumu na zinahitaji umakini, utulivu na mipango sahihi kupata matokeo mazuri. Huu sio muda wa maneno maneno, Ni muda wa vitendo, tena vitendo vya kibingwa," aliongeza Kamwe