Ligi Kuu ya NBC inaendelea leo ambapo mabingwa watetezi Yanga wako mkoani Lindi kuikabili Namungo Fc katika mchezo utakaopigwa uwanja wa Majaliwa, Ruangwa.
Yanga iliwasili mapema jana na jioni ikapata nafasi ya kukamilisha maandalizi yake katika dimba la Majaliwa ambako mchezo huo utapigwa saa 1 usiku.
Ni wazi hautakuwa mchezo mwepesi, Namungo ina historia ya kuwapa wakati mgumu Wananchi kila timu hizo zinapokutana.
Namungo wako nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 20, kinara wa mabao mpaka sasa kwenye ligi ni mshambuliaji wa timu hiyo Fabrice Ngoy aliyepachika mabao 7 katika mechi 14.
Kwa Yanga hii ni mechi muhimu kusaka alama tatu ili kuendelea kujiwekea mazingira mazuri ya kutetea ubingwa wao kwa msimu mwngine.
Wananchi wanashika nafasi ya tatu wakikusanya alama 22 baada ya mechi nane, alama tatu zitawashuhudia wakisogea nafasi ya pili.
Katika mchezo huo Yanga itakosa huduma ya mshambuliaji wake Prince Dube ambaye alipata majeraha katika mchezo uliopita wa kombe la CRDB dhidi ya Cosmopolitan.
Hata hivyo Laurindo Aurelio 'Depu' ambaye amepachika mabao matatu katika mechi mbili za ligi, anatarajiwa kuongoza safu ya ushambuliaji.
Nyota wengine wa Yanga wanaotarajiwa kukosa mchezo huo ni Clement Mzize, Kibwana Shomari, Aboutwalib Mshery, Edmund John na Aziz Andabwile wakikabiliwa na changamoto za majeraha na ugonjwa.