Yanga imetoka kuondoshwa kwenye michuano ya ligi ya mabingwa ikikosa nafasi ya kutinga robo fainali kwenye mechi ya mwisho licha ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JS Kabylie.
Wananchi sasa wanarudi 'mazima' kwenye mashindano ya ndani, kesho Jumatano, Februari 18 wakitarajiwa kushuka dimba la KMC Complex kuikabili Cosmopolitan katika mchezo wa hatua ya 64 bora kombe la Shirikisho la CRDB.
Unaweza kusema ni bahati mbaya kwa Cosmopolitan kwani wanakwenda kukutana na Yanga ambayo imetoka kujeruhiwa.
Pamoja na kuwa mkufunzi wa Yanga Pedro Goncalves anaweza kufanya 'rotation' kwa kuwapumzisha baadhi ya wachezaji waliotumika mfululizo, Yanga bado ina kikosi imara kinachoweza kuisambaratisha Cosmopolitan inayoshiriki ligi ya Championship.
Vijana wa Goncalves watashuka dimbani hapo kesho wakiwa na dhamira ya kuanza michuano ya kombe la CRDB kibabe kwa ushindi mnono.
Yanga ndio mabingwa watetezi wa taji hili wakiwa wamelitwaa kwa misimu minne mfululizo.