Kocha Mkuu wa Yanga Pedro Goncalves amesema maandalizi kuelekea mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya JS Kabylie yamekamilika na anaamini itakuwa nafasi kwa wachezaji wake kuonyesha wako tayari kucheza mechi yenye presha kubwa na kuibuka na ushindi.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari kuelekea mchezo huo ambao utapigwa kesho Jumapili katika uwanja wa New Amaan Complex, Goncalves amesema anatambua hautakuwa mchezo mwepesi lakini wanakwenda kupambana kusaka ushindi.
"JS Kabylie ni timu nzuri na imara yenye uwezo mkubwa ambayo imewekeza kwa kiasi kikubwa msimu huu ili kurejea katika historia ya mafanikio. Tunafahamu vizuri ubora na udhaifu wao."
"Kabylie wanakuja bila presha kwa kuwa tayari wameshatoka kwenye mashindano, lakini bado wataingia uwanjani kwa lengo la kuonesha ukubwa na heshima ya klabu yao. "
"Lakini huu ni muda wetu kuonesha uwezo dhidi ya timu ngumu. Tunapaswa kucheza kwa umakini na tahadhari kubwa malengo yetu yakiwa ni kuibuka na ushindi."
"Tuko tayari na tutakwenda kutimiza majukumu yetu vyema uwanjani, kwa idhini ya Mungu tutafanikiwa kupata pointi muhimu na kufuzu hatua inayofuata," alisema Goncalves.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, beki wa kushoto Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr' amesema wachezaji wote wako tayari kwa mchezo huo, ari na morali yao ikiwa juu.
Zimbwe Jr amesema ni aina ya mechi ambazo yeye huepnda kuzicheza na atakuwa tayari kuisadia timu yake kupata matokeo mazuri na kusonga mbele hatua ya robo fainali.
"Mechi ya kesho ni aina ya mechi ambazo mimi binafsi nazipenda kwa sababu zinakutambulisha wewe ni mchezaji wa aina gani. Binafsi nimejiandaa vizuri na nitashirikiana na wachezaji wenzangu ili kuhakikisha timu ya Wananchi inasonga mbele hatua inayofuata," alisema