Kiungo wa zamani wa Yanga, Stephanie Aziz KI ana matumaini timu hiyo inaweza kuibuka na ushindi mnono dhidi ya JS Kabylie na kujiweka katika nafasi nzuri ya kutinga robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika.
Jumapili, Yanga inashuka saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar, kukabiliana na JS Kabylie katika mechi ya mwisho ya Kundi B ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikisaka tiketi ya kucheza robo fainali kwa mara nyingine baada ya msimu uliopita kukwama kwa MC Alger pia ya Algeria.
Aziz KI ambaye kwa sasa amejiunga na klabu ya Ittihad ya Libya akitokea Wydad CA, amesema presha haipo kwa mashabiki tu hata viongozi kwa na wachezaji kwani lengo ni kuhakikisha wanafuzu hatua inayofuata na siyo kushindwa.
Aziz KI amesema amezungumza na baadhi ya wachezaji wa Yanga na wamemhakikishia kwamba wamekuwa na maandalizi mazuri hivyo hakuna kitakachowakw amisha kupata ushindi nyumbani.
“Nimeongea na baadhi ya wachezaji wa Yanga, wamenihakikishia watafanya kila linalowezekana kuhakikisha Yanga wanapata matokeo yanayohitajika ili wafuzu,” amesema Aziz KI na kuongeza;
“Mashabiki wa Yanga lazima watulie kwani timu yao ilikuwa kundi gumu na bado inaweza kufuzu ikitegemea na matokeo ya Jumapili na wachezaji wa Yanga wanatakiwa kupambania nembo ya timu ili kuendeleza ukubwa wa klabu, ” Ki alinukuliwa na gazeti la Mwanaspoti