Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga Rodgers Gumbo ambaye ameongoza msafara nchini Morocco, amesema maandalizi kuelekea mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya AS FAR yanakwenda vizuri.
Gumbo amesema timu imekuwa na wakati mzuri wa kutimiza maandalizi yake hapo Morocco, ari na morali ya wachezaji ikiwa juu.
"Maandalizi yetu hapa Morocco yanakwenda vizuri. Tangu tuwasili hapa siku mbili zilizopit, hatujakutana na changamoto yoyote kubwa"
"Hali ya hewa sio mbaya sana kwani kumekuwa na vipindi tofauti vya baridi na mvua za hapa na pale lakini niseme tu sio changamoto kwetu"
"Kila mmoja yuko tayari, ari na morali ya timu iko juu kuelekea mchezo wetu siku ya Jumamosi. Ninachoweza kuwaambia mashabiki wa Yanga huko nyumbani sisi tuko tayari, wao watuombee dua ili tuweze kuibuka na ushindi hapo kesho," alisema Gumbo
Yanga chini ya kocha Pedro Goncalves leo itakamilisha maandalizi yake katika uwanja wa Olympic kuelekea mchezo huo utakaopigwa saa 4 usiku kwa saa za Tanzania.
Matokeo ya ushindi kwa Yanga yanaweza kutosha kuwahakikishia Wananchi kutinga robo fainali kutegemeana na matokeo ya mchezo kati ya JS Kabylie dhidi ya Al Ahly.