Kocha Mkuu wa Yanga Pedro Goncalves amesema kikosi chake kimeelekea Morocco huku wakifahamu jukumu lililoko mbele yao katika mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya AS FAR utakaopigwa Jumamosi.
Yanga ilindoka jijini Dar es salaam jana, wakipitia Dubai ambapo leo wanatarajiwa kuwasili huko Morocco.
Akizungumza muda mfupi kabla ya 'kukwea pipa', Goncalves alisema ni mchezo muhimu kwa Yanga ambao watapaswa kucheza kwa tahadhari kubwa, wakiwa na mkakati juu ya aina ya matokeo wanayohitaji.
"Hii ni mechi muhimu kwetu, tunapaswa kuwa makini na kuchukua tahadhari pia dhamira ikiwa kufanikisha malengo ya kufuzu"
"Kama tutapata ushindi tunaweza kufuzu moja kwa moja, lakini hata tukipata sare tutakuwa na nafasi nzuri ya kusonga mbele pia"
"Tukipoteza kwa bao moja bado tutakuwa na nafasi lakini tutaongeza ugumu lakini kama tutapoteza kwa tofauti ya mabao mawili itakuwa tumeondolewa mashindanoni"
"Hivyo kama nilivyosema mwanzo tunakwenda kwa tahadhari lakini tunajiamini, "alisema Goncalves
Kwa lugha nyepesi ni kuwa Yanga itahitaji kushinda au kama alama tatu zitakuwa ngumu basi warudi nyumbani na alama moja ili wamalize kazi kwenye mechi ya mwisho dhidi ya JS Kabylie.