KLABU ya Young Africans (Yanga) bado inabeba hatma yake ya kufuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya matokeo ya michezo ya raundi ya nne ya Kundi B kuendeleza ushindani mkali katika mbio za kusonga mbele.
Yanga ililazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Al Ahly ya Misri katika mchezo uliochezwa jana, matokeo yaliyoifanya ifikishe pointi tano na kuendelea kushika nafasi ya pili katika msimamo wa Kundi B.
Katika mchezo mwingine wa kundi hilo, AS FAR ya Morocco iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JS Kabylie ya Algeria, ushindi uliowafanya kufikisha pointi tano pia, lakini wakabaki chini ya Yanga kutokana na kanuni za Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Kwa mujibu wa kanuni za CAF, timu zinapolingana pointi huangaliwa kwanza matokeo ya ana kwa ana kabla ya kuangaliwa uwiano wa mabao. Yanga inaendelea kuwa juu baada ya kuifunga AS FAR katika mchezo wa kwanza uliochezwa Dar es Salaam.
Matokeo hayo yameufanya mchezo ujao kati ya Yanga na AS FAR, utakaochezwa Jumamosi ijayo Februari 07 nchini Morocco, kuwa na umuhimu mkubwa katika kuamua hatma ya kufuzu robo fainali.
Yanga inaweza kufuzu mapema endapo itaibuka na ushindi nchini Morocco, hasa kama JS Kabylie watashindwa kupata ushindi dhidi ya Al Ahly. Hata hivyo, hata matokeo ya sare ugenini au kipigo kisichozidi mabao mawili, huku wakifunga angalau bao moja la ugenini, yanaweza kuilinda Yanga kutokana na rekodi yao nzuri ya ana kwa ana lakini muhimu watahitaji pia kushinda mechi ya mwisho nyumbani dhidi ya JS Kabylie.
Mchezo huo utachezwa bila uwepo wa mashabiki wa AS FAR, baada ya klabu hiyo kuadhibiwa na CAF, hali inayotarajiwa kuipa Yanga nafuu ya kisaikolojia.
Baada ya mchezo wa Morocco, Yanga itahitimisha hatua ya makundi Februari 13 kwa kuikabili JS Kabylie katika dimba la New Amaan Complex, Zanzibar, ambapo ushindi au matokeo mazuri yatathibitisha rasmi tiketi ya robo fainali.
Kwa hali ilivyo sasa, Yanga bado inabaki kuwa na nafasi kubwa ya kufuzu hatua ya robo fainali, ikiwa kila kitu kikiwa bado mikononi mwao.