Wapinzani wa Yanga wa mchezo wa ligi ya mabingwa, Al Ahly wamewasili visiwani Zanzibar leo kuelekea mchezo baina ya timu hizo utakaopigwa siku ya Jumamosi, Januari 31.
Al Ahly wamewasili nchini bila kiungo wao mahiri Emam Ashour ambaye inaelezwa hakuonekana uwanja wa ndege kuungana na wenzake wakati timu hiyo ikiondoka Misri.
Taarifa kutoka vyanzo vya habari huko Misri, imethibitisha kuwa Ashour ambaye katika mchezo uliopita alikuwa kikwazo kwa Yanga kutokana na umahiri wake katika eneo la kiungo, amesimamishwa kwa muda wa wiki mbili na kupigwa faini. Ni baada ya 'kukacha' safari ya kuja Tanzania na wachezaji wengine.Β

Wakati Al Ahly 'wakivurugana', Yanga inaendelea na maandalizi yake kuelekea mchezo huo leo ikikamilisha siku ya pili ya maandalizi visiwani Zanzibar.
Wananchi hawana muda wa 'kufuatilia' cinema za wapinzani wao, wakijiandaa kukabiliana na kikosi kamili cha mabingwa hao wa kihistora Afrika
Yanga imepania kuzibakisha alama zote tatu visiwani Zanzibar na kujiweka katika nafasi nzuri ya kutinga robo fainali