Baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Al Ahly, Kocha Mkuu wa Yanga Pedro Goncalves amesema wanarejea nyumbani kujipanga ili kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo wa marudiano utakaopigwa wiki ijayo Januari 31 jijini Dar es salaam.
Goncalves amesema waliingia na mkakati mzuri katika mchezo huo lakini ni lazima wakubali wamekutana na timu yenye wachezaji bora ambao wameweza kutumia mapungufu machache yaliyojitokeza katika mchezo huo.
"Timu yetu inakua, binafsi ni mchezo wangu wa kwanza kupoteza hapa, tulihitaji kupata matokeo mazuri lakini haikuwa hivyo"
"Malengo yetu ni kuvuka hatua hii ya makundi na tunaweza kufanikiwa. Hakuna mtu alitupa nafasi baada ya kupangwa kwenye kundi lenye mabingwa wote Al Ahly, AS FAR na Kabylie"
"Tunajua ili tuweze kufikia mafanikio hayo lazima tuzifunge timu kubwa. Haitakuwa rahisi lakini tutapambana," alisema.
Licha ya kipigo hicho, Yanga imeendelea kusalia nafasi ya pili kundi B ikiwa na alama nne huku Al Ahly wakijikita kileleni na alama saba.
Leo JS Kabylie itachuana na AS FAR katika mchezo mwingine wa kundi B.
