Leo majira ya saa 10 jioni Yanga itashuka uwanja wa KMC Complex kuikabili Mashujaa Fc katika mwendelezo wa ligi kuu ya NBC.
Mashabiki wa Yanga wanasubiri kuona kama nyota wao wapya Laurindo Dilson Maria Aurelio maarufu kwa jina la Depu sambamba na Allan Okello, watatumika katika mchezo huo.
Uongozi wa Yanga umefanya jitihada kuhakikisha vibali vya wachezaji hao vinapatikana kwa wakati, huenda leo wakashuhudiwa dimba la KMC Complex.
Nyota wengine wapya Emmanuel Mwanengo na Mohamed Damaro tayari walionekana kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi Yanga ikibeba taji kwakuifunga Azam kwa penalti 5-4.
Okello na Depu wameshiriki kikamilifu mazoezi kuelekea mchezo huo na unaweza kusema wako tayari kuanza kuipigania nembo ya Yanga.

Yanga iliwasajili nyota hao kama wachezaji muhimu kuimarisha maeneo yaliyoonekana kuwa na changamoto eneo la ushambuliaji.
Mchezo dhidi ya Mashujaa Fc leo Yanga inaweza kutumia kama sehemu ya maandalizi kuelekea mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya Al Ahly.
Ni wazi mkufunzi wa Yanga Pedro Goncalves atahitaji kuwatumia nyota hao ili aweze kuona ni kwa kiasi gani wanaweza kuingia katika mfumo wake kwa haraka.