Inaelezwa Yanga inapambana kukamilisha usajili wa mlinda lango wa Pamba Jiji Yona Amos katika dirisha hili.
Tangu msimu uliopita, Yanga ilijaribu kumnasa Amos bila ya mafanikio lakini wakati huu inaonekana mlinda lango huyo usajili wake unaweza kufanikiwa akitarajiwa kuchukua nafasi ya Aboubakar Khomein ambaye mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu.
Khomein amekuwa na wakati mgumu kupata nafasi mbele ya Djigui Diarra na Aboutwalib Mshery ambaye kwa sasa ameshika majukumu kwenye michuano ya kombe la Mapinduzi.
Yona amekuwa katika kiwango bora msimu huu ambapo hata msimu uliopita alishika namba mbili kwa makipa wazawa akiwa na clean sheet 11, nyuma ya Patrick Munthari wa Mashujaa, aliyekuwa nazo 14.
Kocha wa Pamba Jiji Francis Baraza amesema timu hiyo itaongeza nguvu eneo la golikipa ingawa hakuwa tayari kukiri kama Yona anakwenda kujiunga na Yanga
“Hadi sasa hivi tunavyozungumza bado sijaanza kusajili, ila kama ni kuongeza itabidi niongeze beki wa kati kutokana na kuondoka kwa Abdallah Kheri ‘Sebo’, bila hivyo pia mchakato wa beki ya kati ulikuwa unafanyika lakini pia na eneo la kipa"
“Sijataja kuwa Yona anaondoka ila kuna utaratibu wa kuongeza wachezaji katika sehemu nilizotaja kuhusu kipa wetu namba moja kuondoka sina taarifa hizo nasikia kama unavyosikia wewe,” alisema Barazaa
Baraza amesema tetesi zipo, hivyo hawezi kuongelea mchezaji ambaye yupo naye kwenye uwanja wa mazoezini kama biashara itafanyika basi atakuwa kwenye nafasi ya kuzungumza.
“Sasa ni dirisha la usajili mengi yanazungumzwa hivyo kuhusu Yona kuondoka mengi yanasemwa, lakini mimi kama kocha sina taarifa rasmi ila mchakato wa kuongeza mchezaji kwenye nafasi yake unaendelea,” Baraza alinukuliwa na Mwanaspoti