Yanga inahusishwa kumuwania kiungo mshambuliaji wa Vipers na timu ya Taifa ya Uganda, Allan Okello.
Okello yuko katika kikosi cha Uganda Cranes kinachoshiriki michuano ya Afcon 2025 huko Morocco ikiwa kundi C pamoja na Tanzania, Tunisia na Nigeria.
Inaelezwa Rais wa Yanga Injinia Hersi Said anaendesha mchakato wa kumnasa kiungo huyo fundi 'kimyakimya' akimtumia Khalid Aucho, kiungo wa zamani wa Yanga ambaye ni nahodha wa Uganda Cranes.
Okello pia anawindwa na klabu ya Simba ambayo ilijaribu kumsajili katika dirisha lililopita bila ya mafanikio.
Taarifa kutoka ndani ya uongozi imedokeza kuwa mazungumzo ya kumnasa fundi huyo yanaendelea vyema.
“Tunakwenda naye vizuri, unajua Okello ni mbunifu sana licha ya mwili wake mdogo, kama akipatikana itakuwa hatua nzuri kwenye kikosi chetu,” mtoa taarifa alinukuliwa na Mwanaspoti
Mkufunzi wa Yanga Pedro Goncalves amependekeza maboresho eneo la kiungo cha ushambuliaji (namba 10) katika ripoti yake aliyowasilisha kwa uongozi.
Msimu uliopita katika eneo hilo Yanga ilimpoteza Stephane Aziz Ki aliyetimkia Wydad CA huku ikiachana na Clatous Chama aliyejiunga na Singida BS.
Mohamed Doumbia aliyesajiliwa kama mbadala wa Aziz Ki, bado hajathibitisha kulimudu vyema eneo hilo mpaka sasa akiwa hajatoa pasi ya bao wala kufunga.
Mara kadhaa msimu huu Mudathir Yahya ametumika katika eneo hilo hata hivyo nae amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara.