Haikuwa jambo jepesi kwa uongozi wa Yanga kumuondoa kocha Romain Folz ambaye alihudumu kwenye nafasi ya kocha mkuu kwa takribani miezi miwili tu.
Lakini sasa unaweza kumpongeza Rais Injinia Hersi Said na uongozi wake kwani walifanya uamuzi sahihi wakiwasikiliza wanachama walio wengi waliotaka mabadiliko ya benchi la ufundi.
Ujio wa kocha Pedro Goncalves umekuja na mabadiliko yanayoonekana kwenye kikosi cha Yanga na unaweza kusema mwanzo wake umewapa faraja mashabiki na wanachama wa Yanga.
Goncalves ameiongoza Yanga katika mechi nne za mashindano, ameshinda mechi tatu na sare moja.
Ni ushindi katika mechi mbili za ligi kuu, mechi moja ya ushindi kwenye ligi ya mabingwa na sare kwenye michuano hiyo dhidi ya JS Kabylie.
Ingawa bado ni mapema kumpamba Goncalves lakini kazi yake inaonekana, Yanga imebadilika sana.
Kuna mabadiliko ya kimfumo lakini pia hata 'fitness' ya wachezaji inaonekana kuimarika kulinganisha na mwanzo.
Juzi wachezaji wa Yanga walionyesha nidhamu ya hali ya juu katika mchezo dhidi ya JS Kabylie, mechi iliyokuwa na presha kubwa na kufanikiwa kupata alama moja muhimu ugenini, haikuwa rahisi.
Goncalves si kocha muoga, timu yake haichezi soka la kujihami, wanakwenda kushambulia wote na pale wanapopoteza mpira wachezaji wote wanawajibika kwenye kuzuia.