Shirikisho la soka barani Afrika (CAF) limemtangaza mwamuzi Ahmad Imtehaz Heeralall, raia wa Mauritius kuwa ndiye atakayechezesha mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ligi ya mabingwa (CAFCL) kati ya Yanga dhidi ya AS FAR utakaopigwa Jumamosi Novemba 22 katika uwanja wa Benjamin Mkapa.
Haitakuwa mara ya kwanza kwa mwamuzi huyo kuchezesha mechi zinazohusisha klabu za Yanga na AS FAR kwani amewahi kuchezesha mechi mbili za Yanga na moja ya AS FAR.
Katika mechi za klabu, Julai 29, 2018 makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, mchezo ukipigwa kwenye Uwanja wa Mkapa ambapo Yanga ilipoteza kwa mabao 3-2 mbele ya Gor Mahia ya Kenya.
Katika msimu wa 2024-2025, alichezesha mechi ambayo Yanga iliichapa TP Mazembe mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Mkapa, ikiwa ni makundi Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa Januari 4, 2025.
Katika mechi moja aliyoichezesha AS FAR Rabat, timu hiyo ilifungwa mabao 2-0 na USM Alger hatua ya robo fainali Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022-2023.
Refa huyo amechezesha mechi 49 za michuano mbalimbali ikiwamo ya kirafiki ngazi ya klabu na timu za taifa zilizo chini ya CAF na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).