Beki wa Yanga Ibrahim Bacca mapema jana alishindwa kusafiri na kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' kuelekea Misri baada ya kupata changamoto ya kiafya uwanja wa ndege wa Kimataifa JNIA.
Bacca alilazimika kubaki nchini na kurejea kambini Avic Town ambapo baada ya afya yake kuimarika, jioni akashiriki mazoezi ya kikosi cha Yanga kuelekea mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ligi ya mabingwa dhidi ya AS FAR ambao utapigwa Novemba 22 dimba la New Amaan Complex, Zanzibar.
Taifa Stars inatarajiwa kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Kuwait Novemba 14 huko Misri.
Aidha habari njema zaidi kwa Wananchi ni kurejea mazoezini kwa kiungo Mudathir Yahya ambaye alikuwa nje kwa siku kadhaa akiuguza majeraha ya goti.
Mudathir pia alijumuishwa kwenye kikosi cha Stars lakini hakuweza kuungana na wenzake kutokana na changamoto iiyokuwa ikimkabili.
Nyota hao wote walishiriki mazoezi ya Yanga hapo jana ambayo yalifanyika uwanja wa KMC Complex.
Baada ya mchezo wa Stars dhidi ya Kuwait, wachezaji wengine waliokuwa kwenye majukumu ya Stars nao watarejea kuungana wenzao katika maandalizi ya kuikabili AS FAR.
