Yanga imerejea mazoezini kuanza maandalizi ya mchezo wa kwanza hatua ya makundi ligi ya mabingwa barani Afrika dhidi ya AS FAR utakaopigwa Novemba 22 katika uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar.
Kocha Mkuu wa Yanga Pedro Goncalves ana takribani siku 10 za kukiandaa kikosi chake kuelekea mchezo huo ambao Yanga itahitaji kushinda.
Akiwa ameanza vyema majukumu yake ndani ya Yanga akishinda mechi mbili za ligi zilizopita, Goncalves sasa anakwenda kwenye mtihani wake wa kwanza kwenye ligi ya mabingwa.
Jukumu lake ni kuhakikisha anaivusha Yanga hatua ya robo fainali na ili kufikia malengo, alama zote tisa katika mechi za nyumbani lazima zipatikane.
Yanga iko kundi la kifo, kundi lililojumisha timu imara ambazo zina historia ya kufanya vyema katika michuano ya CAF na hata sasa zinafanya vyema katika ligi za ndani, Al Ahly, AS FAR na JS Kabylie.
Yanga inaongoza ligi, Al Ahly na AS FAR zinashika nafasi ya pili huku JS Kabylie pekee ikiwa nje ya tatu bora ikishika nafasi ya 7.
Msimu uliopita AS FAR walitolewa na Pyramids Fc hatua ya robo fainali hivyo ni wazi wameweka malengo makubwa zaidi msimu huu kama ilivyo kwa Yanga ambayo msimu uliopita iliishia hatua ya makundi.
Yanga imechagua kutumia uwanja wa Amaan katika mechi za makundi uongozi ukiamini itawapunguzia wachezaji presha ambayo wamekuwa wakiipata wanapocheza dimba la Mkapa.