Kiungo wa Yanga Mudathir Yahya ameongeza idadi ya majeruhi katika kikosi cha Wananchi kufuatia majeraha aliyopata katika mchezo dhidi ya Silver Strikers.
Mudathir alitumika kwa takribani dakika 24 katika mchezo huo ambao Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 na kutinga hatua ya makundi ya CAFCL.
Tangu apate majeraha hayo, Mudathir hajaonekana tena kikosini ambapo vipimo vya awali vilibainisha ana changamoto ya goti na huenda akahitaji upasuaji
"Tangu ameumia dhidi ya Silver Strikers bado hajarudi, vipimo vya awali vimefanyika ana shida ya goti"
"Amefanyiwa uchunguzi zaidi sasa kinachosubiriwa ni taarifa ya kitaalamu kubaini ukubwa wa jeraha na aina ya matibabu iwe kupata mapumziko ya muda ama kufanyiwa upasuaji kwani mchezaji mwenyewe analalamika ana maumivu makali,” kilieleza chanzo
Mudathir ameendelea kuwa nguzo muhimu katika kikosi cha Yanga msimu huu licha ya ujio wa viungo mahiri katika eneo lake kama Mohamed Doumbia, Lassine Kouma na Moussa Balla Conte. Hata hivyo majeraha hayo yanamfanya asionekane mara kwa mara uwanjani.
Kama atafanyiwa upasuaji huenda Yanga ikamkosa kwa wiki kadhaa na pengine akazikosa mechi za mwanzo za hatua ya makundi ligi ya mabingwa dhidi ya AS FAR na JS Kabylie ambazo zitapigwa mwishoni mwa mwezi huu