Jana ilikuwa siku ya kipekee kwa mshambuliaji wa Yanga Andy Boyeli akifungua akaunti yake ya mabao katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya KMC.
Boyeli aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Prince Dube ambaye bado unaweza kusema anajitafuta, hakuhitaji muda mrefu kuandika bao lake la kwanza kupitia mkwaju wa penati baada ya yeye mwenyewe kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari.
Wakati mchezo ukielekea ukingoni, Boyeli akaweka kamba yake ya pili likiwa ni bao la nne kw Yanga iliyoibuka na ushindi mnono wa mabao 4-1 na kupanda juu ya msimamo kwa mara ya kwanza msimu huu.
Kama ulivyo utamaduni wa mashabiki wa Yanga katika dimba la KMC Complex, Boyeli akapokewa vyema na mashabiki baada ya mchezo wakamtuza 'mapesa'.
"Ninajivunia mashabiki wa Yanga, unajua nimekuwa nikipambana sana tangu wakati wa pre-season, leo nimepata nafasi ya kufunga na mashabiki wamenihamasisha zaidi"
"Mabao haya nimeyatoa zawadi kwa mashabi, nawashukuru sana kwa kuniunga mkono. Niwaambie tu msimu ndio kwanza umeanza na sisi wachezaji wao tutaendelea kupambana ili tuzidi kuwapa furaha," alisema Boyeli.