Jana Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) lilimtangaza Kocha wa Singida Black Stars, Miguel Angel Gamondi raia wa Argentina kuwa Kaimu kocha mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’'
Gamondi amekabidhiwa mikoba ya Hemed Suleiman ‘Morocco’ ambaye mkataba wake umesitishwa kwa makubaliano ya pande mbili.
Taarifa iliyotolewa na TFF ilieleza kuwa mazungumzo yalifanyika kati ya TFF na Singida Black Stars kuhusu Kocha huyo kuchukua majukumu hayo mapya na kubainisha kuwa kocha huyo wa zamani wa Yanga ataiongoza Taifa Stars kwenye Fainali za AFCON zitakazofanyika nchini Morocco kuanzia Desemba mwaka huu.
Gamondi aliiongoza Yanga kwa msimu mmoja na nusu ambapo mafanikio yake yalikuwa kutwaa mataji yote ya ndani yaani Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na kombe la CRDB na pia kuipeleka Yanga hatua ya makundi na robo fainali ya ligi ya mabingwa (CAFCL) baada ya kusubiri miaka 25.
Akiwa na Singida BS msimu huu ametwaa taji la CECAFA pamoja na kuipeleka makundi ya kombe la Shirikisho (CAFCC) kwa mara ya kwanza.
Tanzania iko kundi C katika michuano ya AFCON ikiwa sambamba na Nigeria, Tunisia na Uganda