Baada ya kupoteza mchezo wa mkondo wa kwanza kuwania tiketi ya kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga inarejea Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumamosi ikiwa haina nafasi ya kufeli. Ni lazima washinde kwa angalau 2–0 ili kusonga mbele, hakuna nafasi ya mahesabu mengine. Ni mechi ya maamuzi: wafuzu au wataishia hapa.
Katika mitandao ya kijamii tayari hali imechangamka. Wapo wanaoamini Yanga imeshapotea, huku kampeni kubwa ikiendeshwa na watani wao wa jadi Simba ambao faraja yao ingekuwa kuona mabingwa hao wa Tanzania wakikwama.
Wachambuzi nao hawajabaki nyuma; wanakumbushia kumbukumbu za maumivu fainali ya Kombe la Shirikisho 2022/23 waliyoipoteza nyumbani kabla ya kusawazisha ugenini, pamoja na sare tasa dhidi ya MC Alger iliyowafuta ndoto za robo fainali msimu uliopita.
Historia hizo zote zinatumika kama fimbo ya kukatisha tamaa. Lakini ukweli mwingine upo wazi: hii Silver Strikers ni wageni katika hatua hizi; yenyewe kufika hapa tu ni mafanikio.
Yanga ndiyo wenye shinikizo, timu yenye wachezaji zaidi ya 10 wa timu za taifa, yenye uwekezaji mkubwa na mipango mikubwa ya kutikisa Afrika. Hawa ndio walioujenga msimu huu kwa matarajio ya hatua za juu, si kufa kabla ya makundi.
Mechi ya Jumamosi ni dakika 90 za kuzima kelele zote za mitandaoni. Ni mchezo ambao utatoa hukumu ya kazi nzima ya kocha Patrick Mabedi na kikosi chake. Hakuna matokeo yatakayoitwa “yanatosha” zaidi ya ushindi na kufuzu.
Ndiyo maana Yanga itaingia na mitutu yote kwa sababu hii si mechi ya kuvutia macho, ni mechi ya kuandika mstari mpya kwenye malengo ya klabu.
Presha ipo, ni kubwa lakini Yanga ina wachezaji waliobobea katika mechi za namna hii; waliowahi kuhimili moto mkubwa zaidi ndani na nje ya Afrika.
Jumamosi majibu yote yatapatikana. Haitakuwa tu mechi ya kufuzu, itakuwa jaribio la tabia, utimamu wa timu, na uthibitisho wa kwamba hii Yanga kweli si ya kushindwa kupata nafasi ya makundi. Hii ni do or die kwa Wananchi.