Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga Patrick Mabedi amesema dhamira yake ni kuona mabingwa hao wa nchi wanapata ushindi dhidi ya Silver Strikers siku ya Jumamosi na kufuzu hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa (CAFCL)
Baada ya kupoteza mchezo wa mkondo wa kwanza, Yanga ina mtihani wa kupindua meza nyumbani ikihitaji angalau ushindi wa mabao 2-0 mbele ya mashabiki wake 60,000 wanaotarajiwa kujitokeza dimba la Mkapa siku ya Jumamosi
Mabedi ambaye alikabidhiwa mikoba ya kuinoa Yanga kwa muda wakati mchakato wa kusaka kocha mkuu ukiendelea, amesema wanajiandaa kikamilifu ikiwa ni pamoja na kufanyia kazi changamoto zilizojitokeza katika mchezo uliopita na kupelekea wapoteze
Amesema mchezo wa marudiano utakuwa muhimu zaidi kwao kwa kuwa watacheza nyumbani mbele ya mashabiki wao huku lengo likiwa kuvuka hatua hiyo na kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
"Tuna dakika 90 muhimu nyumbani, mashabiki waje kwa wingi kutuunga mkono. Tumepata muda wa kujiandaa na kufanya marekebisho muhimu kufuatia kile kilichojitokeza katika mchezo wa kwanza"
"Tutarejea uwanjani tukiwa na ari, morali na uchu wa kusonga mbele, nafasi ya kufanya hivyo ipo mikonini mwetu," alisema kocha huyo raia wa Malawi.