Klabu ya Yanga imepokea ombi la Wanachama na Mashabiki wake mchezo dhidi ya Silver Strikers usiwe na viingilio ili mashabiki wapate fursa ya kujitokeza kwa wingi na kuibeba timu yao kuelekea hatua ya makundi
Baada ya uongozi wa Yanga kukutana mapema leo, wameridhia kuondoa viingilio katika mchezo dhidi ya Silver Strikers
Viingilio vimeondolewa kwa majukwaa yote isipokuwa VIP A na VIP B ambapo majukwa yamehifadhiwa kwa ajili ya wageni waalikwa na watu maalum
"Ni ombi ambalo mmelileta Wanachama na Mashabiki wetu na haikuwa rahisi kwa uongozi kuridhia ombi hili"
"Lakini kwa upekee wake, viongozi wamezingatia maslahi ya mapana ya klabu na kuzingatia mchezo huo ni kuipeleka Yanga hatua ya makundi"
"Kwa kuwa wanachama na mashabiki tulipeleka ombi hilo, sasa tuna jukumu la kujaza uwanja wa Benjamin Mkapa, tunakwenda kutengeneza hamasa na shamrashamra za aina yake uwanja wa Benjamin Mkapa. Tunakwenda kuipeleka timu yetu kwenye hatua ya makundi"
"Naomba nisisitize ombi hili ni la wanayanga kwa viongozi wa Yanga, hivyo tunawatahadharisha wale ambao sio wanayanga kuja kuleta vurugu na kufanya chochote kibaya kwa ajili ya timu yetu"
"Hatutazuia shabiki yeyote kuingia uwanjani lakini hatutavumilia wale watakaokuja na ajenda tofauti," alisema Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe
Kamwe amesema Silver Strikers watawasili nchini siku ya Alhamisi saa 2:30 usiku ambapo watafanya mazoezi yao ya mwisho siku ya Ijumaa