Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amewataka wanachama na mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi uwanja wa Benjamin Mkapa siku ya Jumamosi katika mchezo wa mkondo wa pili kuwania tiketi ya kutinga hatua ya makundi ligi ya mabingwa barani Afrika dhidi ya Silver Strikers
Kamwe amesema viingilio vya mchezo huo vimetangazwa mapema na tiketi tayari zinapatikana vituoni na kwenye mitandao ya simu
"Tumetangaza viingilio mapema ili mashabiki muanze kununua tiketi, hii ni mechi muhimu kwetu ni zaidi ya dakika 90"
"Hii sio mechi ya kawaida kwa sababu sote tunapaswa kwenda kuipambania timu yetu ili tuipeleke hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa"
"Inawezekana kabisa kwa umoja, dua, nguvu, sala na sauti zetu ndani ya uwanja wa Benjamin Mkapa, tunao uwezo wa kupindua matokeo"
"Lakini huu uwezo unaanza na wewe Mwanachama na Shabiki wa Yanga. Niwahakikishie wachezaji wanafanya maandalizi kabambe na wako tayari kwenda kuipambania Yanga kwa dakika 90 kuhakikisha tunapata matokeo mazuri dimba la Mkapa," alisema Kamwe
Baada ya kurejea nchini wakitokea Malawi, Yanga leo inaingia kambini kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya mchezo huo ambao Wananchi watahitaji angalau ushindi wa mabao 2-0 ili kuweza kusonga mbele hatua ya makundi