Rais wa Yanga Injinia Hersi Said ameeleza kujivunia mafanikio aliyopata kama kiongozi wa taasisi kubwa ya mpira wa miguu nchini na hata kupata nafasi ya kuaminiwa kuwa Mwenyekiti wa umoja wa klabu Afrika (ACA) na sasa akiteuliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya mashindano ya FIFA
Akizungumza na waandishi wa habari viwanja vya Gymkhana mapema leo, Hersi amesema kile alichofanya akiwa Yanga kimedhihirisha kuwa vijana wanaweza kufanya mambo makubwa pale wanapopewa nafasi
“Kwa Kipekee sana leo ni siku muhimu sana kwangu. Niwashukuru sana wadau mbalimbali waliojitokeza siku ya leo. Nimeona umuhimu wa kuandaa tukio hili kubwa kwangu kwa maslahi mapana ya soka la Tanzania. Tumepitia changamoto mbalimbali wakati tunaingia kwenye mpira lakini kwa namna ya kipekee tumefanikiwa kuvuka”
“Nakumbuka mwaka 2020 Mr Ghalib aliniambia kuwa amealikwa kuichangia klabu. Mwaliko huo ulitokea kwa Antony Mavunde. Hapo ndipo ilikuwa chachu ya mabadiliko makubwa kwa klabu. Tukafanikiwa kushinda zabuni ya jezi. Baadae nikagundua kuwa klabu hii uwekezaji wa jezi hauwezi kuonesha matunda kama klabu inasuasua. Hivyo tukaona umuhimu kuinua klabu kwa kusajili wachezaji. Tukasajili wachezaji wanne. Tukamsajili, Ditram Nchimbi, Haruna Niyonzima, Bernard Morrison.”
“Tuliikuta klabu ipo kwenye wakati mgumu sana. Tukawahamisha hoteli waliyokuwa. Tukawatafutia uwanja mzuri wa mazoezi. Tukaongeza thamani. Lakini tukabaini kuwa gharama ni kubwa sana. Nikamwambia Mr Ghalib tutafute njia mbadala wa malengo ya muda mrefu ambao utaisaidia klabu kujikwamua kuichumi. Wakati ule GSM ndiye aliyekuwa anaisaidia klabu kwenye kila kitu kwa gharama zake. Hivyo tukaona kuna umuhimu wa klabu hii kupunguza utegemezi”
“Baba yangu alikuwa shabiki mkubwa wa Yanga. Nilijitosa kuwania nafasi ya uongozi ndani ya klabu hii kwa sababu nilitamani sana kuisaidia klabu yangu. Nilipata changamoto ya kutokuaminika mwanzoni kwa sababu ya umri. Ilikuwa ngumu kwa kijana wa miaka ya 30 kuchaguliwa kuwa Rais wa Klabu Kongwe. Niwaombe wadau wa soka kuwaamini vijana,” alisema Hersi