Klabu ya Yanga inakamilisha maandalizi kuelekea mchezo wa mkondo wa kwanza kuwania kufuzu hatua ya makundi CAFCL dhidi ya Silver Strikers, utakaopigwa nchini Malawi, Jumamosi ijayo katika uwanja wa Bingu Mutharika, Lilongwe.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema baada ya tathmini waliyofanya, hali Lilongwe kwa sasa ni joto kali hivyo wanajiandaa kukabiliana na mazingira hayo
Kamwe amesema kutokana na hali hiyo, ndiyo maana waliamua kucheza mechi dhidi ya TRA United majira ya mchana, wakati wa jua kali. Ijumaa iliyopita, Yanga ilicheza mechi kwenye Uwanja wa Gymkhana dhidi ya TRA United, iliyoisha kwa suluhu, ulimalizika mchana.
Kamwe, amesema sababu ya kucheza majira hayo ya jua kali ni kutokana na taarifa ya kuwa mchezo wao dhidi ya Silver Strikers, utachezwa saa 10:00 kwa saa za Tanzania, ambapo ni saa 9:00 mchana kwa saa za Malawi muda ambao kutakuwa na joto kali.
"Tulicheza mechi mchana kwenye jua kali kwa sababu tumepata taarifa kuwa huko Malawi kuna joto kali sana, ndiyo maana tulitaka mechi ichezwe kwenye mazingira haya, na kwa bahati nzuri tuliwaambia wenzetu TRA United, wakakubali."
“Katika mchezo ule tulitoka nao suluhu, lakini lengo halikuwa hilo, lengo ni kwamba wachezaji wetu wazoee kucheza kwenye mazingira hayo, tukifika kule tusisumbuke na hali ya hewa na tuwe imara zaidi. Naamini kwa maandalizi haya tutakwenda kufanya vizuri," alisema Kamwe.
Akizungumzia maandalizi upande wa wanachama na mashabiki, alisema mwamko umekuwa mkubwa hasa kwa maeneo jirani ya nchi hiyo, Mbeya na Iringa.
"Niwapongeze wanachana na mashabiki wa Yanga wa Mbeya na Iringa, wameonekana kuhamasika zaidi kwenda nchini Malawi. Dar es Salaam nao naona mwamko umeanza kuwa mkubwa, watu wanajiandaa. Nawasihi Wanayanga, waendelee kujitokeza kwa wingi tukaisapoti timu yetu nchini Malawi, imebakia michezo miwili tu, wa ugenini na nyumbani ili tuweze kutinga hatua ya makundi," alisema Kamwe.
Baada ya mchezo wa Jumamosi, mechi ya marudiano itachezwa, Oktoba 25, mwaka huu, saa 11:00 jioni, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam. Yanga iliingia raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabinmgwa Afrika baada ya kuitoa Wiliete du Benguela ya Angola kwa jumla ya mabao 5-0, ikianza kwa kushinda ugenini mabao 3-0, kabla ya kushinda nyumbani, mabao 2-0, mchezo wa hatua za awali.