Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, yuko nchini DR Congo akishiriki Mkutano wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), akiwa pia katika wadhifa wake kama Rais wa Umoja wa Vilabu Barani Afrika (ACA).
Lakini nyuma ya safari hiyo, macho na masikio ya wanayanga yameelekezwa kwake, wakisubiri uamuzi wake kuhusu hatma ya Kocha Mkuu Romain Folz.
Taarifa kutoka ndani ya klabu zinaeleza kuwa Hersi ndiye mwenye uamuzi wa mwisho kuhusu mustakabali wa kocha huyo ambaye kwa sasa anakabiliwa na ukosoaji mkubwa kutoka kwa mashabiki na baadhi ya viongozi kutokana na kutoridhishwa mbinu zake.
Chanzo cha ndani kimeeleza kuwa mpaka sasa hakuna uamuzi rasmi uliochukuliwa na uongozi wa Yanga, suala hilo litafungwa rasmi baada ya Hersi kurejea kutoka DR Congo.
“Unajua Rais tu ndiye mwenye uamuzi wa mwisho. Wapo wanaopinga kocha na wapo wanaomuunga mkono. Rais amewasikiliza wote, lakini hajatoa uamuzi. Tunamsubiri arudi ndipo tujue kama ataendelea au la,” chanzo kilinukuliwa na Mwanaspoti.
Wakati presha ikiendelea, Folz mwenyewe alitarajiwa kurejea jana Jumapili kutoka mapumziko Afrika Kusini, na leo anatarajiwa kuongoza mazoezi ya Yanga, baada ya mapumziko ya siku tatu kufuatia ratiba ya kalenda ya FIFA.
Kocha huyo raia wa Ufaransa bado ana nafasi ya kuonyesha mwelekeo mpya katika kipindi hiki muhimu, hasa ikizingatiwa mechi zilizo mbele zitaamua hatma ya Yanga kucheza hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa