Tetesi zinazidi kushika kasi kuwa huenda Yanga ikaachana na kocha wake Mkuu Romain Folz baada ya miezi miwili tu tangu ajiunge na mabingwa hao wa nchi
Haitakuwa mara ya kwanza kwa Yanga kufanya mabadiliko ya benchi la ufundi baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa timu kimbinu licha ya kuwa Folz hajapoteza mchezo wowote tangu alipotua Yanga
Mwaka 2020 Yanga ilimfuta kazi Zlatko Krmpotic baada ya siku 37 tu tangu alipojiunga na mabingwa hao wa kihistoria kipindi hicho wakiwa wanaanza kujipanga baada ya kipindi kirefu cha mateso na njaa kali
Baada ya kuachana na Krmpotic Yanga ilimuajiri Cedric Kaze ambaye hata hivyo nae hakumaliza msimu nafasi yake ikichukuliwa na Nasreddine Nabi ambaye mashabiki wa Yanga wanaamini ndio aliyejenga msingi wa Yanga hii ya sasa
Bado hakuna taarifa rasmi kutoka ndani ya uongozi juu ya hatma ya Folz lakini ni wazi kama maamuzi hayo yatafanyika, Yanga italazimika kuajiri kocha ambaye tayari anafahamu mazingira ya kikosi cha sasa cha Yanga
Makocha waliopita Yanga siku za karibuni ndio wenye nafasi kubwa ya kurejea tena kwani athari ya mabadiliko ya kocha wakati huu inaweza kuwa kubwa hasa kama itakuwa mara ya kwanza kwa kocha huyo kufanya kazi nchini
Makocha kama Miguel Gamondi, Sead Ramovic, Miloud Hamdi na hata Nasreddine Nabi wanaweza kuwa chaguo sahihi kwa Yanga wakati huu
Hawa ni makocha ambao hawatahitaji muda mrefu kuirejesha Yanga katika mfumo sahihi wa kiuchezaji hasa ikizingatiwa tangu walipoondoka, kikosi hakina mabadiliko makubwa
Hamdi alimaliza msimu uliopita akitwaa mataji matatu, kama Yanga itamrudisha ni wazi anaweza kuendeleza pale alipoishia kwani kile kikosi chake cha kwanza alichomaliza nacho msimu kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Simba ndicho ambacho Folz amekitumia katika mechi muhimu ikiwemo mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba
Hamdi hana wakati mzuri tangu alipojiunga na Ismailia ya Misri, pengine ni kocha anayeweza kupatikana kirahisi sokoni
Ramovic japo alifanya kazi kwa muda mfupi Yanga, lakini alitambulisha aina ya soka la kasi ambalo liliwapa wakati mgumu timu pinzani. Ile GUSA, ACHIA TWENDE KWAO ilikuwa tayari imeanza kutesa wapinzani Yanga ikifunga mabao mengi chini yake
Lakini utaratibu aliotumia kuondoka pengine ndio utamfanya asiwe pendekezo ndani ya uongozi. Ramovic nae ana wakati mgumu ligi kuu ya Algeria kwani katika mechi tano zilizopita ameshinda mechi moja tu
Gamondi yuko na kikosi cha Singida Black Stars na ameanza msimu kwa kushinda mechi zote mbili. Kocha huyo pia ameingoza Singida BS kutwaa taji la Kagame CECAFA Cup huku a kiivusha Singida BS hatua ya awali ya kombe la Shirikisho (CAF CC)
Nabi yuko nchini kwa siku kadhaa mapumzikoni, yuko nje ya majukumu ya ukocha katika klabu ya Kaizer Chiefs baada ya kuibuka mgogoro baina yake na waajiri wake hao
Pengine ndiye kocha ambaye mashabiki wa Yanga wanatamani zaidi kumuona akirejea kwa mara nyingine kuinoa klabu ya Yanga