Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema wameyasikia maoni ya mashabiki wa timu hiyo mkoani Mbeya ambao hawakufurahishwa na matokeo ya mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mbeya City uliopigwa uwanja wa Sokoine
Yanga imelazimishwa suluhu ya bila kufungana na Mbeya City ambayo pengine ingeweza kuondoka na ushindi dakika za lala salama kama sio uimara wa mlinda lango Djigui Diarra
Baada ya mchezo kumalizika, mashabiki wa Yanga walisikika wakimtupia lawama kocha Romain Folz
"Mchezo ulikuwa mgumu na tumegawana pointi na wapinzani wetu Mbeya City. Tumeyasikia malalamiko ya mashabiki wetu, wametimiza wajibu wao, wamekuja kwa wingi uwanjani na wametoa maoni yao"
"Wao kama mashabiki wametimiza wajibu wao, benchi la ufundi nao wametimiza wajibu na hata uongozi unatimiza wajibu wake. Hivyo tutulie wala tusiwe na haraka," alisema Kamwe
Akizungumza baada ya mchezo huo, kocha mkuu wa Yanga Romain Folz alisema alipata wakati mgumu kuiandaa timu yake kimbinu kutokana na hali ya uwanja
"Kwa kweli ilikuwa ngumu hata kwangu kama kocha, uwanja haukuruhusu mpira kuchezwa, hii ni mara yangu ya kwanza kukutana na mazingira kama haya"
"Wachezaji wangu wamefanya jitihada kubwa, haikuwa rahisi kufunga licha ya kutengeneza nafasi nyingi," alisema Folz