Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imemteua Oscar Mirambo, Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, kuwa Kaimu Katibu Mkuu wa shirikisho hilo kuanzia tarehe 1 Oktoba 2025.
Uteuzi huu unakuja kufuatia kumalizika kwa mkataba wa aliyekuwa Katibu Mkuu, Wilfred Kidao, ambaye atamaliza rasmi majukumu yake tarehe 30 Septemba 2025.
Taarifa ya TFF iliyotolewa mapema leo imethibitisha hatua hiyo, ikiweka wazi kuwa Mirambo ataendelea kusimamia majukumu ya ofisi ya Katibu Mkuu sambamba na nafasi yake ya ufundi hadi hapo utakapofanyika uteuzi wa kudumu.
Mirambo ni jina linalotambulika sana kwenye soka la vijana na maendeleo ya ufundi nchini, ambapo ameongoza program mbalimbali za kukuza vipaji na kuandaa walimu wa soka. Uzoefu huu unatarajiwa kuipa nguvu sekta ya utawala wa TFF.
Msimu uliopita, jina la Wilfred Kidao liliibuka sana kwenye mgogoro uliokuwa kati ya klabu ya Yanga SC na viongozi wa TFF kufuatia mchezo wa namba 184 kati ya Yanga dhidi ya Simba uliopaswa kupigwa Machi 8, lakini uliahirishwa.
Yanga ilipendekeza kuondolewa kwa baadhi ya viongozi akiwemo Kidao, aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Steven Mguto, na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Bodi ya Ligi Almas Kasongo, kama njia ya kusuluhisha mvutano huo. Hatimaye, mgogoro huo ulipatiwa ufumbuzi na mchezo ukachezwa tarehe 25 Juni, ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.