Kocha Mkuu wa Yanga, Romain Folz, ameanza kazi yake kwa kasi ya aina yake, akionesha mapema tu taswira ya kile ambacho mashabiki wa Wananchi wanaweza kutarajia msimu huu.
Akiwa na takribani miezi miwili tangu aingie rasmi Jangwani, Mfaransa huyo ameendeleza pale Yanga ilipoishia msimu uliopita kwa kushinda mataji, huku akianza kuingiza falsafa na mifumo yake taratibu ndani ya kikosi.
Taji la kwanza la Folz liliwasili kupitia Ngao ya Jamii, ambapo Yanga iliichapa Simba kwa bao 1-0 katika pambano lililovuta macho ya wengi wiki iliyopita. Huo ulikuwa mwanzo wenye kuashiria msimu wa ushindani mkali.
Ushindi huo umechafua hali ya hewa kule Msimbazi kwani kilikuwa kichapo cha sita mfululizo na kupelekea kocha wao mkuu Fadlu Davids 'kuingia mitini'
Haikutosha hapo, Yanga pia imeanza vyema kampeni ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikishinda mabao 3-0 dhidi ya Wiliete ya Angola ugenini, matokeo yaliyoiweka Yanga katika nafasi nzuri ya kusonga mbele hatua inayofuata.
Folz amekuja Yanga katika kipindi ambacho timu iko na utajiri mkubwa wa vipaji. Kila eneo lina mafundi wenye uwezo, jambo linalompa nafasi ya kuchagua silaha tofauti kwa kila mchezo.
Kikosi kimeboreshwa zaidi msimu huu, na mapungufu yaliyoonekana awali yametatuliwa kwa usahihi, hali inayofanya iwe vigumu kubaini udhaifu ndani ya timu.
Mafanikio ya msimu uliopita yametengeneza mazingira ya amani na utulivu ndani ya kikosi. Folz ameikuta Yanga ikiwa na morali ya juu, bila presha kubwa, hivyo kazi yake kubwa ni kuendeleza moto huo na kuhakikisha anapandikiza mbinu mpya za kiuchezaji.
Tofauti na makocha wengi wapya, Folz amepata nafasi ya kuona kikosi chake mapema kupitia maandalizi ya msimu (pre-season). Ameona wachezaji karibu wote, akajua wapi pa kuimarisha na namna ya kutumia ubora wa kila mmoja.