Licha ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Wiliete katika mchezo wa mkondo wa kwanza hatua ya awali michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika, Kocha Mkuu wa Yanga Romain Folz amesema bado wana kazi ya kufanya hasa katika matumizi ya nafasi
Folz amesema kama washambuliaji wake wangekuwa makini, walikuwa na nafasi ya kumaliza mchezo huo katika kipindi cha kwanza
"Tumeshinda mabao matatu, ni ushindi mzuri lakini nadhani tungeweza kufanya zaidi. Katika kipindi cha kwanza pekee tungeweza kufunga mabao matatu au zaidi lakini hatukutumia vyema nafasi nyingi tulizotengeneza"
"Ni hivyo hivyo katika kipindi cha pili lakini angalau tulifanikiwa kufunga mabao mawili. Bado ni mapema, tutaendelea kuimarika zaidi, ushindi wa mabao matatu ugenini sio mbaya," alisema Folz
Mshambuliaji Prince Dube pengine ndiye atakayejilaumu zaidi kwa kupoteza nafasi nyingi katika mchezo huo ambao alifunga bao moja huku mabao mengine yakifungwa na Aziz Andabwile na Edmund John
Yanga itahitaji ushindi au matokeo yoyote ya sare ili kusonga mbele raundi ya kwanza