Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) limebadilisha uwanja wa mchezo wa mkondo wa kwanza hatua ya awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Wiliete Banguela dhidi ya Yanga utakaopigwa Septemba 19
Awali, Yanga ilitarajiwa kuanza kampeni yake ya Ligi ya Mabingwa kwa kucheza ugenini dhidi ya Wiliete Benguela ya Angola mjini Benguela Septemba 19, kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo, CAF imeuhamishia mchezo huo jijini Luanda, mji mkuu wa Angola
Hatua hiyo ni ahueni kwa Yanga kwani wangelazimika kusafiri kwa zaidi ya saa nane kwa gari kutoka Luanda kwenda Benguela, au kutumia angalau saa moja kwa ndege.
“Tumepata unafuu mkubwa. Sasa mchezo utafanyika mjini Luanda tofauti na awali ambapo tulipaswa kutafuta tena njia ya kufika Benguela. Hii ni faida kwetu,” kilisema chanzo hicho.
Kwa mujibu wa ratiba, mchezo wa mkondo wa kwanza utapigwa Septemba 19, saa 12 jioni na mechi ya marudiano kupigwa uwanja wa Benjamin Mkapa, Septemba 27, saa 10 jioni
Kabla ya mchezo huo, Yanga inakabiliwa na mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya watani zao Simba ambayo itapigwa kesho Jumanne, Septemba 16 katika uwanja wa Benjamin Mkapa