Kiungo mpya wa Yanga SC, Moussa Balla Conte, amesema amefanya uamuzi sahihi kujiunga na mabingwa hao wa Tanzania na ameahidi kushirikiana vyema na wachezaji wenzake kuhakikisha timu inafikia malengo yake kwa msimu huu.
Conte, ambaye ametua Yanga akitokea klabu ya CS Sfaxien ya Tunisia, aliibua gumzo kubwa kutokana na awali kuhusishwa na mpinzani wa jadi wa Yanga, Simba SC.
Ameanza majukumu yake Yanga kwa mafanikio baada ya kutwaa taji lake la kwanza akiwa na Wananchi nchini Rwanda, ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Rayon Sports katika mchezo wa kirafiki wa Rayon Day.
Kiungo huyo anachukua nafasi ya Khalid Aucho, aliyekuwa kipenzi cha mashabiki, hali ambayo imewafanya baadhi kujiuliza kama ataweza kuimudu nafasi hiyo. Lakini Conte amebainisha kuwa hana presha yoyote kutokana na changamoto hiyo.
“Natambua Yanga ni timu kubwa na kwenye nafasi ninayocheza wamepita wachezaji wengi wakubwa. Lakini hilo halinipi presha kwa sababu sichezi peke yangu, uwanjani tunakuwa 11 na kila mmoja ana nafasi ya kufanya vizuri. Ninaamini tukishirikiana kwa pamoja tutafanya makubwa na kuendelea kuipa furaha Yanga,” alisema Conte.
Mchezaji huyo wa Guinea amesema kikosi cha Yanga kimejaa wachezaji wenye ubora na kiu ya mafanikio, na kwa kushirikiana kwa karibu anaamini timu hiyo itaendeleza historia ya mafanikio barani Afrika.
“Ni muda mfupi tu nipo Yanga lakini tayari nimeona ubora mkubwa wa kila mchezaji. Kwa pamoja tuna nafasi ya kufanya vizuri, hivyo sitazami presha bali ninachukua fursa hii kuonyesha uwezo wangu,” aliongeza Conte.
Conte amejumuishwa kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Guinea kwa michezo ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia, akionyesha hadhi ya kimataifa aliyonayo.
Conte anabaki kuwa moja ya usajili uliozua gumzo kubwa ndani ya dirisha la usajili msimu huu, huku mashabiki wa Yanga wakisubiri kuona namna atakavyoweza kuiongoza safu ya kiungo