Beki kisiki wa Yanga SC na timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars, Ibrahim Hamad maarufu kama "Bacca", ameendelea kuonyesha mshikamano wa kipekee na klabu yake ya zamani, KMKM, licha ya kwa sasa kuwa mali ya Wananchi.
Bacca, ambaye ni mwajiriwa wa KMKM na miezi michache iliyopita alipandishwa cheo kutoka Koplo hadi Sajenti kutokana na nidhamu na kiwango chake bora, ameendelea kushikamana na timu hiyo kwa namna ya kipekee.
Kocha Mkuu wa KMKM, Ame Msime Khamis, amefichua namna Bacca alivyogeuka mlezi wa kikosi hicho, akitoa misaada mbalimbali ikiwemo fedha ili kuhakikisha timu inaendelea kusonga mbele kwenye mashindano.
“Bacca ni mwajiriwa wa KMKM, lakini pia ni mlezi wa timu hii. Tangu ameondoka amekuwa akitusaidia kwa mengi. Sasa tunajiandaa na michuano ya kimataifa ametuma fedha kwa ajili ya kununua vifaa vya maandalizi. Si sahihi kutaja ni kiasi, lakini tunamuishi ndani ya timu licha ya kutokuwepo,” alisema Msime.
Aidha, kocha huyo amesema kuwa mara nyingi Bacca hujumuika na KMKM kufanya mazoezi kila anapokuwa mapumzikoni visiwani Zanzibar, jambo linaloonyesha uhusiano wake wa karibu na klabu hiyo iliyomlea kabla ya kung’aa akiwa Yanga na Taifa Stars.
“Naweza kumuita mlezi wa timu. Mbali na kuwa mchezaji, amekuwa akijitoa sana kwa ajili ya KMKM. Anafahamu tuna michuano mikubwa mbele, ametoa fedha kwa ajili ya vifaa ambavyo anaamini vitatusaidia,” aliongeza