Mshambuliaji hatari wa Yanga SC, Clement Mzize, ndiye mchezaji anayeonekana kuwa "most wanted" kwenye dirisha hili la usajili, baada ya klabu hiyo kupokea ofa nyingi kutoka ndani na nje ya Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Yanga, hadi sasa imepokea ofa saba kutoka klabu mbalimbali zinazohitaji huduma ya nyota huyo. Klabu ya Esperance ya Tunisia ndiyo inayoongoza kwa dau kubwa zaidi la Tsh Bilioni 2.6, lakini bado hakuna makubaliano yaliyofikiwa.
Chanzo cha kuaminika kimeeleza kuwa mabingwa hao wa Tanzania Bara wamesitisha hatua ya kumuuza Mzize, na badala yake wameanza majadiliano ya kuboresha maslahi yake ili kumbakisha klabuni.
Yanga imeweka wazi kuwa malengo yake makubwa ni kufanya vyema katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, hivyo wanahitaji kuwa na kikosi bora chenye wachezaji wenye ubora wa juu.
Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, amewahi kusisitiza katika moja ya mahojiano kuwa kabla ya kumuuza mchezaji wao nyota, hatua ya kwanza ni kumshawishi aendelee kubaki ndani ya kikosi. Ikiwa itashindikana, ndipo klabu itaangalia ofa zilizopo mezani.
Kwa sasa, taarifa zinasema Yanga tayari imefungua majadiliano na Mzize ambapo hatua ya kwanza wamempa ofa mpya ya mshahara na marupurupu mengine. Endapo atakubaliana na masharti mapya, kuna uwezekano mkubwa wa kuendelea kumuona Jangwani akitikisa nyavu katika mashindano ya ndani ikiwemo Ligi Kuu na michuano ya kimataifa.