Rais wa Yanga Injinia Hersi Said ameshinda vita nyingine ngumu kwenye usajili akifanikiwa kumpa mkataba kiungo fundi Moussa Balla Conte raia wa Guinea aliyekuwa akiitumikia klabu ya CS Sfaxien
Unaweza kusema kwa mara nyingine Hersi amefanya 'umafia' kwenye usajili wa kiungo ambaye alikuwa tayari mkononi ana mkataba wa klabu ya Simba
Haikuwa rahisi kumnasa kiungo huyo hasa ikizingatiwa alikuwa chaguo la kwanza la kocha wa Simba Fadlu Davids ambaye alianza harakati za kumsajili tangu mwezi Januari kwenye dirisha dogo
Uamuzi wa kumsajili kiungo huyo ulichagizwa na mahitaji ya Yanga kuelekea msimu ujao ambao Yanga imepania kufanya vyema katika michuano ya ligi ya mabingwa
Wakati huu ambao Yanga inakwenda kuachana na Khalid Aucho, ni faida kumpata Conte ambaye licha ya umri wake mdogo, amepata uzoefu wa kucheza mechi za Kimataifa akiwa na CS Sfaxien na timu ya Taifa ya Guinea
Ukitaka kujua thamani ya mchezaji, angalia kwa kiasi gani klabu zilikuwa zikipigana vikumbo kumsajili. Yanga imemsajili Conte mbele ya Simba, Esperance na Pyramids ambazo hata hivyo ni kama zilichelewa kuingia katika kinyan'ganyiro hicho
Wakati wanatua Tunisia kumuulizia kiungo huyo, GSM alikuwa tayari amelipa pesa yote ya usajili kwa klabu ya Sfaxien wakati Simba walikwama baada ya kuomba walipe dau la usajili kwa awamu mbili
Conte ni kiungo halisi mkabaji, ana sifa zote za kucheza katika eneo hilo. Ni mzuri katika kulinda safu ya ulinzi na ana uwezo wa kuchezesha timu kama ilivyokuwa kwa Aucho
Faida kubwa ya kuwa nae katika nafasi ya Aucho ni kuwa bado ni kijana mdogo ana nguvu na anaweza kutumika katika mechi nyingi pasipo kuwa na changamoto za majeraha ya mara kwa mara