Yanga inatajwa kuwa katika nafasi nzuri ya kumsajili nahodha wa Simba Mohammed Hussein 'Zimbwe Jr' baada ya kumpa ofa nono kuliko ile aliyopewa na klabu yake
Taarifa za ndani zinabainisha kuwa Zimbwe Jr ambaye yuko na timu ya Taifa inayojiandaa na michuano ya CHAN 2024 huko Misri, tayari amekabidhiwa mkataba wa Yanga kilichokuwa kinasubiriwa ni yeye kusaini na kurejesha
Tangu juzi mabosi wa klabu ya Simba walikuwa wakihaha kumshawishi asaini mkataba lakini dau waliloweka mezani halikumshawishi
Inaelezwa juzi alifuta utambulisho wake kama mchezaji wa Simba kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii baada ya mazungumzo na waajiri wake kukosa mwafaka
Jana akihojiwa na EFM, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe alisema Zimbwe Jr ni mchezaji mzuri ambaye kila klabu yenye malengo makubwa inatamani kuwa nae
"Bado sijapewa taarifa kama Mohammed Hussein amesajiliwa au la lakini mimi binafsi nitafurahi kama klabu yangu itamsajili Zimbwe Jr," alisema Kamwe
Katika mapendekezo ya maboresho ya kikosi yaliyoachwa na kocha Miloud Hamdi, alipendekeza kusajiliwa kwa beki mwingine wa kushoto wa kusaidiana na Chadrack Boka