Katika harakati za kujiimarisha kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, klabu ya Yanga inatajwa kuingia sokoni kusaka mlinzi wa kushoto baada ya tetesi za kuondoka kwa Nickson Kibabage anayehusishwa na kujiunga na Singida Black Stars.
Kwa sasa, mlinzi wa kushoto anayetegegemewa zaidi na Yanga ni Chadrack Boka kutoka DR Congo. Boka ameonesha kiwango kizuri tangu ajiunge na klabu hiyo, lakini changamoto za majeraha zimekuwa zikimuweka nje ya uwanja mara kwa mara, hali inayoiweka Yanga katika wakati mgumu linapokuja suala la uimara wa safu ya ulinzi kushoto.
Mara kadhaa msimu uliopita, walinzi wa kulia kama Israel Mwenda na Kibwana Shomari walilazimika kucheza kushoto si kwa sababu ya chaguo la kiufundi, bali kwa dharura.
Kibabage, aliyepaswa kuwa chaguo la pili upande huo, hakuwa katika ubora uliotarajiwa, hali iliyowalazimu benchi la ufundi kubadili mipango.
Tetesi za mitandaoni zinamtaja nahodha wa Simba SC, Mohammed Hussein 'Zimbwe Jr', kuwa kwenye rada za Yanga. Inaelezwa kuwa Zimbwe Jr hajatia saini mkataba mpya na Simba, licha ya mkataba wake kumalizika.
Upana wa kikosi ni kipaumbele cha kwanza kwa Yanga hivyo inahitaji kusajili mlinzi ambaye ataleta ushindani katika nafasi hiyo kama ilivyo kwenye nafasi nyingi ambazo Yanga ina machaguo ya mchezaji zaidi ya mmoja
Yanga haitaki kutegemea mchezaji mmoja katika nafasi hiyo nyeti, hasa ikizingatiwa msimu mrefu na mashindano mbalimbali kama CAF Champions League, FA Cup, na Ligi Kuu.
Kumsajili mlinzi wa kushoto mzawa mwenye uwezo wa kupambana nafasi ya kwanza si tu kutampa Boka changamoto ya kuongeza bidii, bali pia kuwa na mchezaji wa kuaminika atakapokosekana