Klabu ya Yanga SC inaendelea na mchakato wa kusaka kocha mpya atakayerithi mikoba ya Miloud Hamdi, aliyeondoka hivi karibuni na kutua katika klabu ya Ismaily ya Misri.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwezi huu wa Julai, jina la kocha mpya litakuwa tayari limetangazwa, na ataanza kazi rasmi katika pre-season itakayoanza mapema mwezi Agosti.
Katika majina yanayotajwa sana kwenye mchakato huu, jina la kocha wa zamani wa Mamelodi Sundowns na Wydad Casablanca, Rulani Mokwena, limekuwa likizungumzwa kwa uzito mkubwa huku kukiwa na taarifa za uhakika kwamba Yanga tayari imewasiliana naye. Hata hivyo, jina jipya limeibuka na kuvutia hisia za mashabiki – kocha wa ASEC Mimosas, Julien Chevalier.
Julien Chevalier ameinoa ASEC Mimosas kwa zaidi ya misimu minne, na amejijengea sifa ya kuwa na falsafa ya soka la kuvutia, lenye kasi na ubunifu. Kinachomtofautisha Chevalier ni uwezo wake wa kuibua vipaji na kuvipeleka viwango vya juu hata bila kuwa na kikosi kilichojaa majina makubwa.
Katika kipindi chake ASEC, Chevalier amefanikisha mafanikio makubwa ikiwemo kufika hatua za makundi, robo fainali na nusu fainali katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho akiwa na wachezaji vijana waliotoka kwenye akademi ya klabu.
Yanga SC imewahi kunufaika moja kwa moja na kazi ya Chevalier. Baadhi ya wachezaji wake nyota waliowahi kucheza chini ya kocha huyo katika ASEC ni pamoja ni, Stephane Aziz Ki, Pacome Zouzoua, Yao Kouassi na Celestin Ecua ambaye tayari ameripotiwa kumalizana na Yanga kwa msimu ujao
Kama kuna kocha anayeweza kuendeleza falsafa ya Yanga, kusajili vipaji na kuvikuza ndani ya mfumo wa kisasa basi huyo ni Julien Chevalier. Kiwango chake cha mafanikio ASEC kinatosha kumpa nafasi ya kujaribu changamoto mpya katika klabu kubwa kama Yanga SC.