Klabu ya Yanga SC leo imefanya ziara maalum ya kutembeza mataji matano waliotwaa katika msimu wa 2024/2025 kwa wadhamini wao wakuu, ikiwa ni ishara ya shukrani na kuthamini mchango wao mkubwa katika mafanikio hayo ya kihistoria.
Ziara hiyo ilihitimishwa kwa kishindo katika Makao Makuu ya kampuni ya GSM yaliyopo Salamander Tower, ambako Mdhamini/Mfadhili wa klabu hiyo, Ghalib Said Mohammed ‘GSM’, alipokea kwa heshima mataji hayo.
Katika msimu huu uliomalizika, Yanga ilibeba mataji matano ambayo ni:
-
Ligi Kuu Tanzania Bara
-
Kombe la CRDB
-
Kombe la Muungano
-
Ngao ya Jamii
-
Toyota Cup
Mafanikio haya hayakuja kwa bahati nasibu. GSM ameendelea kuwa nguzo kuu ya mafanikio ya Yanga kwa kuhakikisha timu inakuwa na wachezaji wa kiwango cha juu, wanaopata mishahara mizuri na kwa wakati. Uwekezaji wake si tu wa kifedha bali pia wa kiutawala, umekuwa uti wa mgongo wa muundo imara wa klabu.
Ziara ya kutembeza mataji ilianza kwa kutembelea ofisi za SportPesa, NIC, na Azam Media, wadhamini ambao pia wamekuwa na mchango mkubwa kwa njia mbalimbali. Kila mmoja alipata fursa ya kushuhudia heshima ya kile ambacho ushirikiano wao umefanikisha.
Hata hivyo, kilele cha ziara hiyo kilikuwa kwenye makao ya GSM, ambapo furaha na fahari vilitawala. GSM alipokea mataji hayo kwa bashasha, akisisitiza kuwa mafanikio ya Yanga ni matokeo ya mshikamano, nidhamu, na mipango madhubuti.




