Kocha Mkuu wa Klabu ya Yanga, Miloud Hamdi, amefurahishwa na ari ya timu yake baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Dodoma Jiji katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliopigwa jana kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, Hamdi aliwapongeza wachezaji wake kwa kupambana na kufanikisha ushindi huo muhimu, licha ya kuanza kwa kusuasua kipindi cha kwanza.
"Niwapongeze wachezaji wangu kwa ushindi huu muhimu. Tulitarajia mechi haitakuwa nyepesi na kipindi cha kwanza Dodoma Jiji walitupa wakati mgumu," alisema Hamdi.
Kocha huyo alieleza kuwa mabadiliko ya kiufundi yaliyofanywa kipindi cha pili yalizaa matunda na kumfurahisha kwa namna ambavyo wachezaji wake waliweza kutekeleza kwa ufasaha maelekezo waliyopewa katika mazoezi.
"Tulibadilika kipindi cha pili. Nimefurahishwa na jinsi kila mchezaji alivyopambana. Tuliwapa nafasi kina Mkude, Farid, na Shekhan, wote wakacheza vizuri sana. Kila mmoja ni muhimu katika timu hii," aliongeza.
Hamdi pia hakusita kuwapongeza mashabiki wa Yanga waliokuwa uwanjani kwa kujitokeza kwa wingi na kuisapoti timu yao.
"Mashabiki ni sehemu ya mafanikio haya. Huu ushindi ni wao, wamekuwa nasi kila hatua, na wana kila sababu ya kushangilia," alisema kwa furaha.
Kwa sasa, Yanga itaendelea kuwepo visiwani Zanzibar kujiandaa na mtanange unaosubiriwa kwa hamu dhidi ya watani wao wa jadi, Simba SC, mchezo utakaochezwa Jumatano, Juni 25 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Ushindi dhidi ya Dodoma Jiji umeiweka Yanga katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu, ikiwa na pointi 79 kileleni mwa msimamo, wakati Simba ikifuata kwa pointi 78. Yanga sasa inahitaji sare au ushindi dhidi ya Simba ili kutwaa taji hilo kwa mara nyingine.