Bodi ya Ligi (TPLB) wakati wowote ikitarajiwa kutangaza taarifa nyeti na muhimu kuhusu mchezo namba 184 ligi kuu ya NBC kati ya Yanga dhidi ya Simba, Wananchi wametulia wakisubiri hatua zitakazochukuliwa na Bodi hiyo
Yanga haijabadilisha chochote katika msimamo wake, kabla ya kukubali kucheza mechi hiyo katika tarehe nyingine (sio Juni 15) ni lazima Mtendaji Mkuu wa Bodi na Katibu Mkuu wa TFF wajiuzulu pamoja na kuvunjwa kwa Kamati ya saa 72
Akizungumza na Azam Media jana, Afisa Habari wa Bodi ya Ligi Karim Boimanda alisema wakati wowote bodi itatangaza taarifa 'nyeti na muhimu' ambayo inakwenda kuhitimisha mchakato mzima wa maandalizi kuelekea mchezo huo
Pamoja na kuweka msimamo kuhusu mchezo huo, Yanga pia ilitangaza hatua ambazo itachukua endapo masharti yake hayatazingatiwa
Yanga haitakwenda uwanjani kucheza dhidi ya Simba Juni 15, lakini pia kwa kuwa haina imani na Bodi ya ligi haitakwenda uwanjani kucheza mechi mbili zitakazofuata dhidi ya Tanzania Prisons na Dodoma Jiji na zaidi haitakuwa tayari kushiriki ligi kuu msimu ujao hadi mabadiliko yafanyike
Aidha Wananchi pia kama hawatalipwa fedha zao za ubingwa wa kombe la CRDB walilotwaa msimu uliopita, hawatacheza mchezo wa fainali dhidi ya Singida Black Stars uliopangwa Juni 28