Zimesalia siku tatu kabla ya mchezo namba 184 wa Ligi Kuu ya NBC kati ya Yanga SC dhidi ya Simba SC, mchezo uliopangwa kufanyika tarehe 15 Juni 2025. Badala ya maandalizi ya uwanjani, macho na masikio ya wadau wa soka nchini yameelekezwa kwenye mvutano mkubwa kati ya Yanga SC na Bodi ya Ligi (TPLB)
Yanga, licha ya kuongoza ligi na ikiwa imefuzu fainali ya CRDB Federation Cup, imesimama kidete kudai mabadiliko ya msingi yanayoonekana kuelekea kwenye ujenzi wa mfumo huru, wa haki na wenye uwajibikaji katika uendeshaji wa soka la Tanzania.
Wapo wanaohoji kwa nini Yanga, timu iliyopo kileleni mwa msimamo wa ligi, iwe na sababu ya kupinga ratiba au kupigania mabadiliko ya uongozi ndani ya TFF na TPLB? Wengine wameenda mbali zaidi wakibeza juhudi hizi kama usumbufu usio na msingi.
Lakini hoja kuu ya Yanga si kuhusu kushinda mechi au kubeba ubingwa, ni kuhusu kusimamia misingi ya haki, utawala bora na heshima kwa kanuni zilizowekwa. Wanasema: hatuwezi kufumbia macho kasoro za wazi kwa sababu tu tunafanya vizuri uwanjani.
Yanga wanapigania kuwepo kwa Bodi ya Ligi iliyo huru, kujiuzulu kwa viongozi wanaotajwa kushindwa kutenda haki, na kuvunjwa kwa Kamati ya Saa 72 ambayo wanaituhumu kwa uamuzi tata unaokiuka taratibu. Haya si madai ya faida binafsi, bali ya kimfumo yanayogusa mustakabali wa ligi nzima.
Yanga imekataa kuwa sehemu ya mfumo ambao unaendeshwa kwa maamuzi ya upendeleo au bila kuzingatia haki, hata kama klabu nyingine zimeamua kunyamaza.
Ifahamike Yanga SC haipambanii tu vikombe, bali misingi ya uongozi bora. Wakati klabu nyingine zinaweza kuona ni vyema "ku-relax" na kuzoea hali ilivyo, Yanga inasema hapana soka linahitaji kulindwa, hata kama una nafasi ya kutwaa taji.
Mashabiki wa soka nchini wanapaswa kuelewa kuwa mjadala huu si wa Yanga peke yake. Ni mjadala wa kila mdau wa soka anayetaka kuona ligi ya Tanzania inapata heshima, uwazi, na maendeleo ya kweli.