Klabu ya Kaizer Chiefs kutoka Afrika Kusini imeamua kuachana na mpango wa kumsajili kipa namba moja wa Yanga SC, Djigui Diarra, baada ya kubaini kuwa mchezaji huyo bado ana mkataba wa miaka miwili na mabingwa hao wa Tanzania Bara.
Taarifa zinaeleza kuwa kocha wa sasa wa Chiefs, Nasreddine Nabi, ambaye pia aliwahi kuinoa Yanga, alitembelea Tanzania hivi karibuni, na ujio wake ulihusishwa na mazungumzo kuhusu usajili wa baadhi ya wachezaji akiwemo Djigui Diarra
Hata hivyo, juhudi za Chiefs zimegonga mwamba baada ya uongozi wa Yanga kuweka wazi kuwa Diarra bado yupo kwenye mkataba mrefu ambao umebakisha miaka miwili. Awali, Chiefs walidhani kuwa mchezaji huyo amebakiza mwaka mmoja, hali ambayo ingewafanya wawe na nafasi nzuri ya kumsajili kwa gharama nafuu.
Mmoja wa viongozi wa juu ndani ya Kaizer Chiefs amenukuliwa na Mwanaspoti;
“Diarra kuna mapendekezo yalikuja ili tumpate, lakini tuliambiwa amebakiza mwaka mmoja. Tulipowasiliana na Yanga, walituonyesha kuwa mkataba wake bado una miaka miwili. Kwa hiyo tunaona itakuwa ngumu kumpata kwa bei rahisi.”
“Tunaweka nguvu kwenye machaguo mengine ambayo tulikuwa nayo. Hatuwezi kuendelea na dili la Diarra. Ni kipa mzuri, lakini bajeti inatuzuia,” alisema kiongozi huyo.
Kwa sasa, inaonekana Djigui Diarra huenda akaendelea kusalia Jangwani kuwatumikia mabingwa hao wa nchi