Katika anga ya soka la Tanzania, jina la Duke Abuya linazidi kushika kasi kama moto wa kifuu. Kiungo huyu fundi raia wa Kenya ameonesha kiwango cha juu msimu huu, na jitihada zake hazijapita bila kuonekana.
Kwa sasa, taarifa kutoka ndani ya mabingwa wa kihistoria, Yanga SC, zinathibitisha kuwa klabu hiyo imeamua kumpa mkataba mnono baada ya mchango wake mkubwa ndani ya kikosi cha kocha Miloud Hamdi.
Abuya alichukua nafasi ya kiungo mkabaji Khalid Aucho wakati alipokuwa nje kwa majeraha, na alifanya kazi hiyo kwa ustadi wa hali ya juu. Wakati mashabiki na wachambuzi walitarajia pengo kubwa, Abuya alijitokeza kama mkombozi, akicheza kwa nidhamu, akili, na maono ya kipekee uwanjani.
Kwa uwezo wake wa kupiga pasi sahihi na kufunika eneo kubwa la kiwanja, alihakikisha Yanga inaendelea kuwa bora katika eneo la kiungo
Hali hii ilimvutia kocha Hamdi kiasi cha kumwaminisha zaidi. Katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la CRDB dhidi ya JKT Tanzania, licha ya Aucho kuwa amepona, Hamdi alimuanzisha Abuya
Tetesi zinadai pia klabu ya JS Kabylie ya Algeria inatajwa kutaka huduma yake, jambo lililowasukuma Yanga kuharakisha mazungumzo ya kuongeza mkataba wake.
Mkataba wake wa sasa unamalizika mwishoni mwa msimu huu, lakini kwa mujibu wa vyanzo vya ndani ya klabu hiyo ya Jangwani, tayari mazungumzo ya kuongeza mkataba mrefu zaidi yanaendelea vizuri.