Rais wa Yanga Injinia Hersi Said ameshiriki kuzindua 'Match of the Legends' mchezo utakaowakutanisha wachezaji wakongwe wa soka visiwani Zanzibar watakaovaana na mastaa wa zamani wa Brazili
Tukio la uziwanduzi wa mchezo huo limefanyika leo Alhamisi visiwani Zanzibar, Golden Tulip Hotel
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi, Hersi alimpongeza Rais wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi kwa juhudi zake za kuendelea kuitangaza Zanzibar duniani
"Nichukue fursa hii kumpongeza Rais wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi kwa juhudi zake za kuendelea kuitangaza Zanzibar duniani"
"Hili tukio la 'Match of the Legends' tunalolizindua leo naamini ni tukio kubwa na la kihistoria kuwahi kufanyika katika ardhi hii. Tunakwenda kumpokea mmoja wa wachezaji bora kuwahi kucheza mpira duniani, Ronaldinho Gaucho akiwa na wenzake"
"Dhamira ya Klabu yetu ya kushiriki kwenye ‘Match of the Legends’ ni kuongeza thamani ya tukio hili. Tutashikiri kwa asilimia mia moja kwenye kufanya promotion na kutoa baadhi ya watendaji wa klabu yetu kuja kusaidia uratibu wa mechi yenyewe"
"Niwaalike Watanzania wote, lakini na rafiki zetu wapenda mpira kutoka sehemu mbalimbali Barani Afrika kuja Zanzibar kushuhudia tukio hili la kihistoria. Naamini kila mpenda soka atapenda kumuona Ronaldinho na wenzake wakicheza soka huu ukiwa umeketi jukwaani," alisema Hersi
Mechi ya kimataifa ya kirafiki baina ya wachezaji hao wa zamani wa Brazili wakiongozwa na Ronaldinho dhidi ya wale wa Zanzibar itafanyika Julai 27 katika Uwanja mpya wa Amaan kuanzia saa 2:00 usiku
Kwa mujibu wa Balozi wa Heshima wa Brazil wa Zanzibar, Abdulsamad Abdulrahim, mechi hiyo itawakutanisha wachezaji maarufu duniani akiwemo Ronaldinho Gaucho na wengine wa zamani kutoka Brazili, huku Zanzibar ikitarajiwa kuongozwa na Abdallah Juma Alley (Abdulwakati Juma), Murtala Ahmad Kibamba, Bakari Masoud, Nassoro Mwinyi Bwanga na wengineo
Abdulrahim amesema, nyota wote wa zamani kutoka Brazil watawasili Zanzibar Julai 26 watafanya mazoezi na vijana wenye vipaji vya soka visiwani humo.